The United Republic of Tanzania Ministry of Health Southern Zonal Referral Hospital

Media Center

MGANGA MKUU WA SERIKALI ATEMBELEA HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA KUSINI ARIDHISHWA NA HUDUMA YA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe leo tarehe 09 Septemba, 2025 ametembelea Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini na kuridhishwa na huduma zinazotolewa kupitia Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Mama Samia wanaoendelea kutoa huduma  za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya ngozi, macho, meno pamoja na magonjwa ya watoto. 


Dkt. Magembe alipata nafasi ya kuzungumza na wanachi waliokuja kupata huduma kupitia kambi hiyo ambapo amesema kuwa mpango wa Serikali ni kuona huduma za madakari Bingwa na Bingwa Bobezi ziwe zinapatikana katika Hospitali mbalimbali nchini na kuongezea kuwa serikali inaendelea kuweka utaratibu wa madaktari bingwa kutoa huduma za Kibingwa mara kwa mara.


Akifafanua maoni ya mteja kuhusu gharama za matibabu, Dkt. Magembe amesema kuwa Serikali imepitisha sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kuwapunguzia gharama za matibabu na kwamba bima hizo zitatumika kupata huduma kuanzia ngazi ya zahanati mpaka hospitali ya Taifa na kuongezea kuwa serikali itatoa elimu kwa wananchi  ili waweze kujiunga na bima ya afya   
“sheria ya bima ya afya kwa wote inakuja kuwa suluhisho la kuhudumia huduma za afya ambapo kila mtanzania atakuwa na bima yake itakayomuwezesha kupata huduma katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya” Dkt. Magembe.


Kupitia ziara yake hiyo, Dkt. Magembe alipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbaliya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na chumba cha kuchuja damu (Dialysis) ambapo aliridhishwa na huduma hizo huku akiwasisitiza wananchi wa ukanda wa kusini wenye changamoto za figo waweze kuitumia huduma hiyo.
“kwa sasa mwananchi yeyote anayeishi ukanda wa Kusini mwenye changamoto ya figo wala haitaji tena kusafiri safari ndefu kwenda Muhimbili kufuata huduma ya kusafisha figo kwasababu huduma hiyo inapatikana katika hospitali yetu ya kanda kwaiyo tuendelee kuitumia hospitali hii“ alisisitiza Dkt. Magembe.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Kusini Dkt. Herbert Masigati amefafanua kuwa kambi hiyo inahusisha magonjwa ya ngozi, macho, kinywa na meno pamoja na magonjwa ya watoto na kuongezea kuwa tayari wagonjwa zaidi ya 350 wamepata huduma kupitia kambi hiyo siku ya kwanza ambapo kati yao wagonjwa wa macho wamekuwa ni wengi zaidi.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameshukuru kwa uwepo wa madaktari Bingwa na wameiomba Serikali kuendelea kuwaleta madaktari bingwa mara kwa mara kwani uwepo wao unawapunguzia gharama za usafiri kwenda Muhimbili na Hospitali zingine kufuata  matibabu ya Kibingwa na Bingwa Bobezi.